Skip to content

Mwenge kumurika miradi ya 140.6bn/- Mjini Magharibi

NA MWANDISHI WETU

MIRADI 23 yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 140.6 inatarajiwa kutembelewa na mwenge wa uhuru unaoanza mbio zake leo katika mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Akitoa taarifa kwa vyombo vya Habari ofisini kwake jana, mkuu wa mkoa huo, idrissa kitwana Mustafa alieleza kuwa baadhi ya miradi hiyo itazinduliwa, kuwekewa mawe ya msingi na kukagua na wakimbiza mwenge kitaifa wanaoongozwa na kiongozi wa mbio hizo Godfrey Eliakimu Mzava.

Kitwana alifafanua kuwa, katika miradi hiyo sita inapatikana katika wilaya ya Magharibi ‘B’, 10 wilaya ya Mjini na saba ya wilaya ya Magharibi ‘A’ ikihusisha sekta mbali mbali zikiwemo za elimu, afya ya jamii na uhifadhi wa mazingira.

“Miradi yote ina thamani ya Shilingi 140,608,956,044.99 ambapo wilaya ya Magharibi ‘B’ ina miradi yenye thamani ya shilingi 59,081,632,352, Mjini, shilingi 27,539,296,770.42 na Magharibi ‘A’, shilingi 53,988,026,921.57”, alieleza Kitwana.

Alifafanua kuwa fedha za miradi hiyo zinatoka katika vyanzo mbali mbali ikiwemo michango ya wananchi (shilingi 3,209,660,425), Michango ya Manispaa (shilingi 41,920,900), michango ya serikali kuu (shilingi 94,236,573,635.99) na michango ya wahisani (shilingi 43,120,801,084).

Aidha Mkuu huyo wa mkoa aliwaomba wananchi, viongozi mbali mbali wa serikali, vyama vya siasa, viongozi wa majimbo na wadi na Jumuia Zisizo za Kiserikali kujitokeza kwa wingi katika mapokezi ya mwenge yatakayofanyika katika Uwanja wa Ndege wa kimataifa wa Abeid Amani Karume leo na maeneo yote ambayo mwenge huo utafika.

 Vile vile aliwakumbusha viongozi wa wizara na taasisi za serikali, wakurugenzi wa manispaa pamoja na viongozi wa vikundi ambao miradi yao itapitiwa na mwenge kuwepo katika maeneo ya miradi ili kutoa maelezo ama ufafanuzi kuhusu midari hiyo pale itakapohitajika.

Aidha aliwashukuru wadau mbali mbali kwa kujitokeza kuchangia mbio hizo ambazo baada ya kupokelewa zitaanza katika wilaya ya Magharibi ‘B’ kabla ya jumamosi kuhamia katika wilaya ya Mjini na jumapili utakuwa katika wilaya ya Magharibi ‘A’ ambapo kwa jumla utakimbizwa umbali wa kilomita 104 kwa wilaya zote tatu.

Aidha aliwahakikishia wananchi wa ndani na nje ya mkoa huo kuwa hali ya ulinzi na usalama itaimarishwa katika maeneo yote ya mkoa hasa yatakayokuwa na mikesha ya mwenge ili kuwapa fursa ya kusheherekea mwenge huo wenye ujumbe usemao ‘Tunza Mazingira na Shiriki katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa Ujenzi wa Taifa Endelevu’.