NA MWANDISHI WETU, OMKR
MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, amekutana na viongozi pamoja na watu mashuhuri kutoka taasisi na mataifa mbali mbali wallioshiriki wa mkutano wa dunia kuhusu utalii, uchumi wa buluu, bahari na mazingira, Jijini Almeria, nchini Hispania.
Katika hafla hiyo iliyofanyika ndani ya ukumbi wa Jiji la Almeria liliopo kusini mwa Hispania, Othman alijumuika na watu mashuhuri katika chakula cha usiku, kilichoandaliwa na Baraza la Kimataifa la ‘Sun and Blue’ ambapo alipata nafasi ya kubadilishana mawazo na uzoefu juu ya kutumia sekta ya uchumi wa buluu na utalii kuimarisha uchumi wa mtu mmoja mmoja na nchi kwa ujumla.
Hafla hiyo iliyoongozwa na Meya ya Jiji la Almeria, Maria del Mar Vasquez Aguero ililenga Kuwakutanisha na kuwatambulisha baadhi ya viongozi na wakuu wa misafara, kutoka maeneo na mataifa mbali mbali duniani waliohudhuria mkutano huo.
Mbali na kushiriki hafla na mkutano huo, Othman alitembelea maeneo mbali mbali yakiwemo majengo ya kihistoria ya ALCAZABA yaliyopo katika mji wa kale wa Andalusia yaliyowahi kukaliwa na Utawala wa Dola ya Uthmaniyya (Ottoman Empire) hadi karne za 18 na 19.
Pia Makamu wa Rais na ujumbe wake, walitembelea maeneo maalum ya utalii unaozingatia vigezo vya mazingira kwa mujibu wa mpango wa kimataifa (Blue Flag) jijini Almeria, Kusini mwa Hispania akiongozwa na wenyeji wa maeneo hayo mashuhuri duniani, wakiwemo Kaimu Mdhibiti wa Majengo ya Urithi ya Andalusia, Maria Angeles Cuena Ramos, Alvaro Casares na Luis Gil ambao ni Wakurugenzi kutoka Mpango wa Kimataifa wa ‘New Eco Planet.
Akitoa salamuzake wakati wa ziara hiyo, alieleza kuwa urithi wa kihistoria popote duniani, siyo tu kuwa ni utambulisho wa nchi au taifa husika, bali pia ni kichocheo na njia muhimu ya kujikwamua kiuchumi.
Alieleza kuwa hiyo inatokana na ukweli kwamba urithi huo ni njia ya moja kwa moja ya kuimarisha sekta ya utalii ambayo imeleta tija na maendeleo makubwa kwa nchi nyingi duniani ambazo baadhi yao zinawiana kwa kiasi kikubwa na Zanzibar au Tanzania.
Akitilia mkazo suala la utunzaji na usafi wa mazingira kwa ajili ya utalii, kupitia uimarishaji wa maeneo ya historia alisema; “Hii tunaichukua kwetu kama ni elimu na fursa kubwa ambayo itatusaidia katika eneo la mazingira na la Utalii, ili tuendane na kasi ya mafanikio katika sekta hizi muhimu za uchumi”.
Kwa upande wake, Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar, Mudrik Ramadhan Soraga, alisema serikali inahitaji kutafakari kuona ni kwa namna gani inaweza kuitumia fursa ya uzuri wa asili wa mandhari ya Zanzibar ili kufanikisha yale ambayo mataifa makubwa ikiwemo Hispania yamepitia ili kukuza uchumi wa nchi.
Ujumbe huo katika ziara hiyo uliongozwa na Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa, anayehudumu pia Hispania, Ali Jabir Mwadini, wameweza kuliona eneo la historia katika mji wa kale wa Andalusia, ambalo miaka ya hivi karibuni lilitelekezwa na kugeuzwa jaa la takataka na maficho ya wahalifu bali sasa baada ya uwekezaji wa takriban Euro Milioni 30, limerudi tena kuwa ni kivutio kikubwa cha utalii.
Pamoja na eneo hilo, walijionea Minara ya Majeshi ya Sultani wa ‘Ottoman Empire”, Mahamamu, Ngome za Warumi, Maeneo yaliyotumiwa na Watawala Majabari, katika Karne Nyingi zilizopita Kihistoria.
Othman aliyewasili nchini Hispania Novemba 18, mwaka huu katika hafla na ziara hiyo aliambatana na mkewe, Mama Zainab Kombo Shaib, Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar, Mudrik Ramadhan Soraga, Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa anayehudumia nchi ya Hispania, Balozi Ally Jabir Mwadin, maafisa a serikali ya mapiduzi Zanzibar na ubalozi pia alieleza namna sekta za uchumi wa buluu na utali zinavyoweza kusaidia nchi kustawisha mazingira na historia zao.