Skip to content

Serikali yaongeza siku 5 maombi ajira za Polisi

  • Bara

SERIKALI imeongeza siku tano kwa Watanzania wanaoomba nafasi za kazi kwenye Jeshi la Polisi na kwamba kama hali ya intaneti itaendelea kuwa na changamoto, itaangalia cha kufanya.

Hatua hiyo ya serikali inakuja kutokana na hapo awali ilitangaza tarehe ya mwisho ya kutuma maombi ni leo lakini imeamua kuongeza muda huo kutokana na changamoto iliyojitokeza ya kimtandao kutofanyakazi vizuri.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni, akitoa ufafanuzi kuhusu taarifa iliyotolewa bungeni na Mbunge wa Makete, Festo Sanga aliyetumia kanuni namba 54 ya kutoa jambo la dharura bungeni.

Kanuni hiyo inamruhusu mbunge kuliomba Bunge kusimamisha shughuli zake na kujadili suala la dharura na kwa mujibu wa Sanga, ukosefu wa mtandao wa intaneti nchini umesababisha vijana wengi kushindwa kuingia kwenye mtandao wa Polisi kuomba ajira hizo.

Mwenyekiti wa Bunge, Deo Mwanyika ametoa mwongozo wa hoja hiyo kwa kuitaka Serikali kutoa maelezo ndipo, Waziri Msauni, amelieleza Bunge kuwa baada ya kutokea tatizo la itaneti nchini wameamua kuongeza siku tano kuanzia kesho.

Masauni pia amesema iwapo changamoto ya intaneti itaendelea,Serikali itaangalia namna ya kufanya ili kuwasaidia waombaji kufikia malengo.

Alisema serikali imeliona tatizo hilo na juzi walikaa na taasisi husika kulifanyia kazi suala hilo, na wamekubaliana kuongeza siku tano na ni vyema vijana wakaendelea na mchakato wa kuchangamkia fursa hiyo.

Alisema siku hizo zitaanza kufanyakazi baada ya zile za awali kumalizika ambapo leo ndio ilikuwa siku ya mwisho, lakini watakaa na kuangalia kwa pamoja kama huduma hizo zitaimarika na namna watavyoweza kuchukua hatua.

Pia, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye naye amelieleza Bunge kuwa mategenezo ya mtandao wa intaneti hadi sasa yako asilimia 80 na kwamba hadi mchana itakuwa imetengemaa kwa asilimia 100.

Mei 9, 2024 Jeshi la Polisi lilitangaza ajira nafasi mbalimbali za ajira kwa vijana wenye elimu ya shahada, astashahada, kidato cha sita na cha nne, huku moja ya sifa kwa muombaji lazima awe raia wa Tanzania wa kuzaliwa.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi makao makuu Dodoma Mei 9,2024, miongoni mwa nafasi hizo kwa upande wa shahada ni 74, diploma 66 na upande wa ngazi ya cheti (astashahada ni 66).

Fani zinazotakiwa kwa kila ngazi ya elimu ni pamoja na uuguzi, famasia, uhandisi wa vyombo vya majini, kompyuta, muziki, wapima ardhi, usimamizi wa michezo na utawala.

Waombaji hao wanatakiwa waandike barua kwa mkono na wasisahau namba za simu na wanapaswa kutumia anuani ya Mkuu wa Jeshi la Polisi S.L.P 961 Dodoma.

Waombaji wote wametakiwa wafanye maombi kupitia kwenye mfumo wa ajira wa Polisi (Tanzania Police Force -Recruitment Portal) unaopatikana kwenye tovuti ya jeshi hilo ya; www Polisi.go.tz na mwisho wa kupokea maombi hayo ni Juni 16, 2024,” ilieleza taarifa hiyo.

Sifa zinazotakiwa kwa mujibu wa taarifa hiyo, sifa nyingine muombaji awe amehitimu wa kidato cha nne na sita kuanzia mwaka 2018 hadi 2023.

Taarifa hiyo imetaka kwa waombaji waliohitimu kidato cha nne, sita na wenye stashahada wawe na umri wa kuanzia miaka 18 hadi 25.

Wale wa kidato cha nne wawe na ufaulu wa daraja la kwanza hadi daraja la nne na ufaulu wa alama 26 hadi 28.

Kwa waombaji wa kidato cha sita wawe na ufaulu wa daraja la kwanza hadi daraja la tatu. Wahitimu wa shahada au stashahada wawe na umri kuanzia miaka 18 hadi 30.

Pia waombaji wawe na urefu usiopungua futi tano na nchi nane (5’ 8”) kwa wanaume na futi tano nchi nne (5’4”) kwa wanawake, wanapaswa kuwa na utambulisho kutoka Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) na awe na uwezo wa kuongea kwa ufasaha lugha ya Kiswahili na Kiingereza.

“Anapaswa kuwa na afya njema kimwili na kiakili iliyothibitishwana daktari wa Serikali na awe hajaoa/kuolewa au kuwa na mtoto.Taarifa hiyo pia ilieleza wenye ‘tatoo’ hawahusiki, kwani imetaka asiwe na alama za kuchorwa mwili (tatoo), asiwe na kumbukumbu ya uhalifu na kwa waombaji wenye elimu ya kiwango cha shahada (NTA levo 8) Shahada (NTA levo 6) na astashahada level (NTA levo 5 au NVA level 3) wanatakiwa wawe na fani zilizoanishwa kwenye tangazo hilo,