Skip to content

Serikali yasaka mwekezaji mwengine wa bandari

  • Bara

DODOMA

SERIKALI inaendelea na taratibu za kumpata mwekezaji mwingine atakayekuwa na jukumu la kufanya shughuli za uendeshaji kuanzia Gati Namba 8 hadi 11 katika Bandari.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Wizara ya Uchukuzi Makame Mbarawa, wakati akiwasilisha hotuba ya Bajeti ya Wizara hiyo kwa mwaka wa Fedha 2024/2025, huko Bungeni Mjini Dodoma.

Waziri huyo alisema lengo ni kuongeza tija katika utendaji wa bandari ili kuziwezesha zichangie zaidi katika ukuaji wa uchumi wa Taifa na maendeleo ya wananchi kwa ujumla.

Alisema Serikali kupitia Wizara ya Uchukuzi imeendelea kushirikisha sekta binafsi katika uendeshaji wa Bandari ya Dar es Salaam kwa baadhi ya maeneo ya bandari kwa kuingia ubia na Kampuni Binafsi katika kuendeleza na kuendesha shughuli za bandari kuanzia Gati Na. 4 hadi 7. Alisema kwa sasa hatua mbalimbali zikiwemo za makabidhiano na ‘mobilization’ zinaendelea ili kuruhusu utekelezaji rasmi kuanza.

Kuhusu Bandari ya Bagamoyo, alisema Serikali imekamilisha zoezi la kulipa fidia kwa wananchi wanaopisha eneo la 55 mradi lenye ukubwa wa hekta 887.

Alisema kwa sasa mradi huo upo katika hatua za mwisho za ukamilishaji wa kuhuisha Upembuzi Yakinifu na Ujenzi wa Bandari hiyo ni wa kimkakati kwa kuwa itachochea shughuli za viwanda na biashara katika eneo la Ukanda Maalum wa Kiuchumi (Special Economic Zone).

Alisema  Serikali kupitia Ofisi za TPA zilizo nje ya nchi imeendelea kufanya jitihada kubwa za kimasoko katika kujitangaza na kutafuta fursa zaidi za kibiashara kwa nchi jirani zinazotumia Bandari za Tanzania zikiwemo nchi za Rwanda, Burundi, Uganda, Zambia, Malawi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Zimbabwe.

Alisema kutokana na jitihada hizo shehena ya 58 mizigo iliyosafirishwa kwenda nchi jirani imeongezeka hadi kufikia tani 8,871,438 kwa mwaka 2023 kutoka tani 8,239,112 kwa mwaka 2022 sawa na ongezeko la asilimia 7.67. 82.

Alisema Serikali kupitia TPA imeendelea kuratibu ununuzi wa vifaa na mitambo kwa ajili ya kuboresha utoaji wa huduma katika Bandari nchini.

Alisema  Hadi kufikia Machi 2024, TPA imefanikiwa kununua na kupokea vifaa na mitambo 121 sawa na asilimia 53.78 ya lengo la kununua mitambo na vifaa 225, Ununuzi wa mitambo hii umeongeza ufanisi katika kutoa huduma bandarini.

Alisema kutokana na umahiri katika utoaji wa huduma za hali ya hewa, mwaka 2019 Shirika la Hali ya Hewa Duniani liliichagua Tanzania kupitia TMA kuendesha kituo cha kanda cha kutoa mwongozo wa utabiri wa hali mbaya ya hewa (Regional Specialized Meteorological Centre) kwa nchi zilizopo katika ukanda wa Ziwa Victoria.

Alisema Kituo hicho kipo Dar es Salaam na kinahudumia nchi tano (5) ambazo ni Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, na Burundi.

Sambamba na hilo, TMA iliteuliwa kutekeleza jukumu la kufuatilia ubora wa takwimu za hali ya hewa (data) zinazopimwa katika vituo vya hali ya hewa vya nchi sita (6) vya ukanda wa Afrika Mashariki ikujumuisha nchi ya Sudan Kusini.

Alisema Majukumu haya ambayo TMA imeendelea kuyatekeleza kwa ufanisi na kuzidi kuitangaza nchi kimataifa.

Waziri huyo aliliomba Bunge kumpitishia bajeti ya makadirio, mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2024/25 ya Wizara ya Uchukuzi kiasi cha shilingi trilioni 2.729 kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na Utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo. 

Alisema kati ya fedha hizo, Shilingi 114,744,476,000 ni kwa ajili ya Matumizi ya kawaida na Shilingi 2,614,931,941,000 ni kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.