Skip to content

‘Tumieni mbegu bora kuongeza uzalishaji muhogo’

NA SALAMA MOHAMED, WKUMM

MKURUGENZI wa Idara ya Utafiti wa Kilimo, Salma Omar Mohamed amewashauri wakulima wa mazao ya muhogo watumie mbegu bora za muhogo ili kuweza kuzalisha kwa wingi na kuongeza kipato

Salma alieleza hayo katika shamba la utafiti wa kilimo Kizimbani,  wilaya ya Magharib ‘A’ Unguja wakati wa zoezi la uvunaji wa mbegu za muhogo zinazostahamili maradhi ya michirizi ya kahawia.

Alisema zoezi hilo lina lengo la kuwapatia wakulima mbegu bora inayostahamili maradhi ya michirizi kahawia ambayo imekua ni changamoto katika uzalishaji wa zao hilo.

Aliongeza kua zao la muhogo ni muhimu kwa wananchi na ni zao kuu tegemezi katika Uhakika wa chakula sambamba na uwepo wa ustahamilivu mkubwa juu ya mabadiliko ya hali ya hewa.

Alisema kwa Zanzibar sasa zao la muhogo limekua na matumizi Makubwa na limezidi kuongeza Thamani ikiwemo upikaji wa chips, makwaru pamoja na kusagwa  kwa  unga kwa ajili ya ugali na uji.

“Niwaombe wakulima wa zao hili tunapokupeni mbegu za muhogo jitahidini sana kuzitunza na kuzipanda kwa ajili ya kuongeza uzalishaji ambao utakaosaidia katika kujipatia mafanikio yatakayotuwezesha kwa ajili ya kujikimu katika maisha yetu”, aliongea Salma.

Kwa Upande wake Mtafiti kutoka Taasisi ya Kimataifa ya Kilimo cha Mazao ya nchi za Kitropiki (IITA), Edda Mushi, alisema sehemu kuu ya utafiti huo ni kuangalia mbegu zenye ukinzani au ustahimilivu mkubwa wa maradhi ya michirizi kahawia na batobato pia zina uzazi mkubwa zaidi.

Hata hivyo Edda alifahamisha hatua hiyom pia ianalenga kupata takwimu sahihi juu ya uzalishaji wa zao hilo kwa mazingira ya Unguja

Na kwamba zoezi hilo kuwashirikisha wakulima kutoka katika wilaya mbali mbali kunawezesha kupata maoni yao juu ya matokeo ya utafiti wa mbegu hizo.

 “Maoni ya wakulima na watumiaji wa mbegu hizi ni muhimu sana kwa tafiti za sasa na hata baadae kwani sifa za mbegu hizi huwa zinatofautiana”, alieleza Edda.

Akizungumza katika hafla hiyo Afisa Kilimo wa wilaya ya Kusini Unguja, Mudathiri Mwinyi Hassan, alitoa wito kwa wakulima wa muhogo kutumia zoezi hilo kuwa fursa katika kuongeza uzalishaji wa zao hilo na mbegu katika maeneo yao na kuzisambaza kwa wakulima wenzao.

Naye mmoja ya wakulima wa muhogo kutoka Dunga Kiembeni, Daud Ramadhan Mwinyi akizungumza kwa niaba ya wakulima wenzake aliishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuanzisha Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (ZAR)I inayosaidia kutatua changamoto zinazowakabili katika shughuli zao.

Aidha  Daudi alitoa wito kwa watafiti wa mazao ya mizizi kuendelea zaidi kufanya utafiti ili waweze kuwapatia taarifa muhimu na matokeo ya upatikanaji wa aina mpya za mbegu.