Skip to content

Tutachukua hatua kutekeleza mkakati usalama barabarani – Hemed

  • Zanzibar

NA MWANDISHI WETU, OMPR

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kuchukua hatua mbali mbali pamoja na kutekeleza mkakati wa usalama barabarani mwaka 2020 – 2030 ili kuondoa vifo visivyokuwa na lazima na ulemavu wakudumu kwa wananchi unaosababishwa na ajali za barabarani.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla , alieleza hayo katika kilele cha maadhimisho ya kwanza ya wiki ya usalama barabarani na uzinduzi wa mkakati wa usalama barabarani Zanzibar katika viwanja vya maonesho Nyamanzi Zanzibar.

Alisema kuwa kila mmoja  ana jukumu la kuhakikisha ajali za barabarani zinapungua na kuondoka kabisa kwa kuchukua tahadhari mbali mbali ili kuepuka madhara yatokanayo na ajali hizo ikiwemo vifo na ulemavu wa kudumu.

Aliongeza kiuwa tafiti zinaonesha kuwa chanzo kikubwa cha ajali za barabarani zinatokana na makosa ya kibinaadamu yanayosababishwa na madereva kutokufuata sheria za usalama barabarani, kutembea kwa mwendo kasi, ulevi, kutumia simu wakati wanaendesha magari, ubovu wa magari, uchakavu wa miundombinu ama hali ya hewa.

Aidha alisema kuwa takwimu zinaonesha kuanzia  mwaka 2019 hadi 2023 jumla ya ajali za barabarani 1,181zimeripotiwa  kwa vyombo husika zilizosababisha vifo 799 na majeruhi 1,461 ambapo kuanzia mwezi Januari hadi Oktoba 2024 ajali 193 zimeripotiwa na kusababisha vifo 264 na majeruhi 216.

Aliiagiza Kamati ya Kitaifa ya Uaalama barabarani kuendelea kutekeleza majukumu yao ya kisheria ikiwemo kutoa elimu ya usalama barabarani kwa jamii na kulitaka Jeshi la Polisi kuendelea  kuhakikisha sheria za usalama zinafuatwa kikamilifu na kuwachukulia hatua wale wote wanaokwenda kinyume na sheria hizo.

Hemed pia aliwataka madereva  wa vyombo vya usafiri barabarani kufuata sheria na kuhakisha uimara wa vyombo vyao kabla ya kuingia barabarani na kuwasihi wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa kwa vyombo vinavyosimamia usalama barabarani kwa kutoa taarifa wanapogundua madereva wanaokwenda kinyume na sheria.

Nae Waizi wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Dk. Khalid Salum Mohammed, alisema ajali za barabarani ni janga la taifa linaloendelea kupoteza maisha ya wanachi, kupata ulemavu wa kudumu, pamoja na upotevu wa mali zao kupanda kwa gharama za matibabu jambo ambalo limekuwa ni  changamoto kubwa kwa wanaopatwa na  majanga ya ajali za barabarani.

Dk. Khalid alisema mashirikiano ya pamoja yanahitajika katika kuhakikisha kila mmoja anafuata sheria za usalama barabarani, kutolewa elimu ya matumiza salama ya barabara ili kumaliza kabisa jangla ajali za barabarani.

Alifahamisha kuwa katika harakati za kupambana na kupunguza ajali za barabarani lazima kuwepo na mazingatio ya mipango miji kwani wimbi la ujenzi holela hasa pembezoni mwa barabara limekuwa likiongezeka jambo ambalo linachangia kuongezeka kwa ajali za barabarani

Kwa upande wake Kamishna wa Polisi Zanzibar, CP Hamad Khamis Hamad,  alipongeza juhudi zinazoendelea kuchukuliwa  na Rais Dk.  Hussein Mwinyi za kuleta maendeleo hasa katika Sekta ya Miundombinu ya Barabara na kuakisi dhamira yake ya kuimarisha Usalama Barabarani na kutokomeza kabisa ajali zinazosababishwa na madereva, wamiliki na wananchi kutokufuata sheria za Usalama barabarani.

CP Hamad alisema kikosi cha Usalama barabarani kinakabiliwa na changamoto mbali mbali ikiwemo watumiaji wa barabara kutokuwa na elimu ya usalama barabarani hivyo ameshauri kuendelea kutolewa elimu kwa wananchi juu ya matumizi bora ya barabara na kufuata sheria za usalama barabarani.

CP Hamad alisema madereva wengi wamekuwa hawafuati sheria pindi wanapokuwa  barabarani  na kusababisha ajali zinazogarimu maisha ya watu na mali zao hivyo amaeshauri kutumika kwa Teknolojia ya kisasa ili kudhibiti mwendo kasi na kuwatambua wavunjifu wa sheria  za usalama barabarani na kuchukuliwa hatua kali za kisheria ili iwe fundisho kwa wengine ambao hufanya makosa kama hayo.

Akizungumza kwa niaba ya wadhamini wengine wa hafla hiyo, Awena Rajab Moh’d kutoka Shirika la Mawasiliano Zanzibar (ZICTIA) alisema ongzeko la ajali limekuwa janaga la Taifa ambapo hatua za dharura zilipaswa kuchukuliwa ili kudhibiti janga hilo ambalo linaendelea kuteketeza maisha ya wananchi wengi nchini.

Alisema ZICTIA inaamini kuwa elimu iliyotolewa katika wiki ya usalama barabarani imewafikia walengwa na itatotoa matokeo chanya hasa katika kufuata sheria za usalama barabarani bila shuruti na kuachana na yale yote yanayopelekea uvunjifu wa sheria na kusababisha vifo, ulemavu wa kudumu na kupotea kwa mali za wananchi.