Skip to content

Wanaotuhumiwa kujihusisha na wizi wa pikipiki mbaroni

JESHI la Polisi Mkoa wa Kusini Unguja, linawashikilia watu wanne kwa tuhuma za wizi wa pikipiki uliotokea kwenye maeneo ya mikusanyiko ya watu.

Akizungumza na waandishi wa habari huko Tunguu Makao Makuu ya Polisi Mkoa wa Kusini Unguja, Kamanda wa Polisi Mkoa huo, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, SACP Daniel Shillah jeshi hilo katika operesheni zake limefanikiwa kuwatia nguvuni watuhumiwa hao.

Kamanda Shillah aliwataja watuhumiwa hao ni pamoja na Iddi Abdalla Kisumba (20), Rashid Abdalla Sadala (19) wakaazi wa Kidimni, Faki Kassim Khamis (19) mkaazi wa Amani na Ahmed Amour Abdalla (24) mkaazi wa Makunduchi.

Alisema katika siku za hivi karibuni kumekuwa na matukio ya wizi wa pikipiki na vyombo vyengine vya moto hasa kwenye mikusanyiko mbalimbali ya watu ikiwa pamoja harusi, misiba na nyumba za ibada.

“Kumekuwa na tabia ya vijana kujihusisha na vitendo vya wizi hasa pale watu wanapokuwa kwenye mikusanyiko hasa mazishi, wakati mwengine vyombo vinaibiwa watu wanapoegesha vyombo vyao wanapokuwa katika harusi”, alisema Kamanda huyo.

Kamanda Shillah alisema watuhumiwa hao wamekamatwa katika matukio tofauti wakiwa na pikipiki tatu zinazosadikiwa kuwa ni wizi walioufanya katika maeneo tofauti.

Katika tukio jengine, Kamanda Shillah alisema wamefanikiwa kuwakamata watu wengine watatu wanaotuhumiwa kujihusisha na unyanganyi wa kutumia silaha.

Kamanda huyo alisema watuhumiwa hao wanadaiwa kuwavizia watembea kwa miguu huwatishia kwa mapanga na kuwapora kisha kukimbia kwa kutumia pikipiki.

Alisema watuhumiwa waliokamatwa ni pamoja na Khalid Salum Said (20), mkaazi wa Fuoni, Yassir Abdalla Shaaban (30), mkaazi wa Fuoni na Ali Mohamed Ali maarufu kama shetani kiro (28) mkaazi wa Kizimkazi Mkoa wa Kusini Unguja.